Tanzania na Angola zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya biashara kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinakazokidhi mahitaji ya watu, soko la kikanda na kimataifa.
Hayo yamesisitizwa wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) alipokutana na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka nchini Angola ukiongozwa na Bw. António Duarte Gomes, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi ya TEGMA-SU LDA ya nchini Angola.
Aidha, katika mazungumzo hayo Mhe. Kombo amesisitiza kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Angola katika kuongeza uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa kufuatia uboreshaji wa miundombinu unaoendelea kutokea ushoroba wa Robito, kupitia Zambia hadi Bandari ya Dar es Salaam kwa reli ya TAZARA utakaorahisisha usafirishaji wa bidhaa, huduma na watu kutoka bahari ya Atlantiki kuja bahari ya Hindi.
Pia, amesisitiza umuhimu wa Tanzania na Angola kuwekeza katika usafiri wa anga ili kuwa na usafiri wa moja kwa moja kati ya nchi hizi mbili utakaorahisisha shughuli za usafirishaji.
Waziri Kombo ametumia nafasi ya mazungumzo hayo pia kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara ambapo ameeleza kuwa kwa upande wa Zanzibar kuna fursa nyingi za uwekezaji kwenye utalii. Kadhalika, amesisitiza umuhimu wa kushirikiana katika sekta ya kilimo pamoja na madini.
Naye, Bw. Gomes amemshukuru Waziri Kombo kwa ukaribisho na ushirikiano wanaoendelea kuupata. Wakiwa nchini ujumbe huu utatembelea eneo ambalo Baba wa Taifa wa Angola Hayati António Agostinho Neto aliwahi kuishi enzi za harakati za ukombozi wa Taifa hilo na Afrika kwa ujumla.
Tanzania na Angola zimekuwa zikishirikiana tangu enzi za harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na hata baada ya kupatikana kwa uhuru, hivyo ushirikiano wa mataifa hayo umeendelea kukua na kuimarika katika masuala yakisiasa, kijamii na hata kiuchumi.