Na Ada Ouko,Musoma.
MFUMO mpya wa kielektronic unaotumika kuendesha Mashauri mbalimbali katika Mahakama kuu kanda ya Musoma umefanikiwa kupunguza gharama kwa wananchi ambapo hawana ulazima wa kufika mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi zao.
Hayo yamebainishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo Fahamu Mtulya February 3 mwaka 2025 wakati akifunga maadhimisho ya wiki na siku ya sheria katika uwanja wa Mahakama hiyo ambayo yalihudhuriwa wadau mbalimbali wa sheria mkoani Mara.
"Mahakama ya Tanzania imeanzisha mifumo ya kielektroniki ambapo mtu anaweza akawa Rorya akafungua shauri Mahakama kuu kanda ya Musoma bila kusafiri, Shauri linaweza likatolewa uamuzi bila mhusika kuwepo kiuhalisia anafuatilia kila kinachoendelea hata kama yuko nje ya nchi"
Katika kutekeleza malengo makuu ya Dira ya taifa ya mwaka 2050 ,mfumo huo unairahisisha mashauri kusikilizwa kwa wakati hivyo kumuondolea mwananchi gharama ya kusafiri na kupoteza muda wa kufanya shughuli zake za maendeleo.
Sambamba na hilo, alisema Mahakama nchini imedhamiria kutekeleza mlolongo wa dira ya maendeleo ya mwaka 2050 kwa kuanzisha vituo jumuishi vya Mahakama ili kusogeza huduma hiyo kwa wananchi.
"Kabla ya mwaka 2019 Mahakama kuu kanda ya Musoma haikuwepo, wananchi wa mkoa wa Mara walikuwa wanalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 240 kwenda Mwanza kupata huduma endapo wakishindwa mashauri kwenye mahakama za wilaya, hilo lilikuwa likimpotezea mwananchi muda na fedha zake alizotumia kama nauli na malazi" alisema Mtulya.
Kwa upande wake Muwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ,Wakili wa serikali Kitia Turoke alisema kila ofisi hiyo inatenga fedha ili kuharakisha matokeo yanayokusudiwa katika dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2050
"Ni jukumu la mwanasheria mkuu wa serikali kuhakikisha anatoa ushauri wa kisheria ambao utasaidia serikali na taasisi zinazosimamia haki madai malengo makuu ya dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2050 yanaweza yakafikiwa ikiwa kila raia atapata haki yake bila vikwazo" alisema.
Muwakilishi wa mkuu wa mkoa ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi mkuu wa wilaya hiyo Juma Chikoka alitoa shukrani kwa muhimili huo wa Mahakama katika kuendelea kushirikiana kuwahudumia wananchi kwa amani na utulivu.
Alisema ametenga muda wa siku mbili, mbili, wa kutekeleza majukumu yake kwa wananchi kwenye halmashauri mbili anazozihudumia za Musoma mjini na Musoma vijijini na kwamba siku moja ni kwa ajili ya kusikiliza kero na kuzitatua akiwa pamoja na watalaamu husika.