Siku ya tarehe 27 Januari 2025, kwenye sherehe ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, *Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF)* chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Wanu Hafidh Ameir (Mb) iliandaa matembezi maalum ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
MIF iliandaa matembezi katika Kiwanja cha Ofisi ya Sheha wa Shehia ya Kizimkazi Dimbani Kusini Unguja kwa lengo la kuwashajihisha wananchi kuimarisha Afya na kupambana na maradhi nyemelezi ambayo yamekuwa yakienea kwa kasi nchini.
Katika matembezi hayo, MIF ilishirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar Pamoja na Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI) katika zoezi la uchangiaji wa damu na upimaji wa moyo kwa wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja Kizimkazi Dimbani ambapo maadhimisho hayo yalifanyika.
Aidha, Mhe. Wanu Hafidh Ameir (Mb) na Mwenyekiti wa Taasisi ya MIF alisema kuwa Kauli Mbiu ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni "MOYO WANGU MAISHA YANGU" inayolenga kuwafahamisha wananchi kutunza afya zao dhidi ya maradhi yasiyoambukizwa.
Vilevile, Taasisi ya MIF ilitoa msaada wa magari manne (4) ya kubebea wagonjwa (Ambulance), ambapo gari mbili ni kwa Hospitali za Unguja na na gari mbili zitapelekwa Pemba; Na Viti hamsini (50) kwaajili ya watu wenye mahitaji maalum.
Mgeni Rasmi katika kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuwa ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, ikihudhuhuriwa na viongozi wengine wa nchini Zanzibar akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Ayoub M. Mahmoud, Waziri wa Afya wa Zanzibar Pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma.
viongozi waliohudhuria waliipongeza Taasisi ya MIF kwa kuendelea kuwekeza katika harakati za maendeleo hasa katika kumuinua Mwanamke kiuchumi, kuimarisha Afya ya jamii na kuokoa vifo vya mama wajawazito na matatizo mbalimbali.




