Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza limedhamiria kufanya operesheni kali ya kubaini na kukamata watu wanaofanya ramli chonganishi na kuchochea uhalifu ikiwemo mauaji yatokanayo na imani za ushirikina.
Hayo yamebainishwa na kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafugwa wakati wa kikao kazi na waganga, wakunga wa tiba asilia pamoja, maafisa wa wanayapori (TAWA) na wadau mbalimbali kilichofanyika katika Bwalo la Polisi Mabatini.
Pamoja na mambo mengine, Kamanda Mutafugwa amewaonya baadhi ya waganga wanaojihusisha na upigaji wa ramli chonganishi na kusema Jeshi la polisi halitasita kuchukuwa hatua kali za kisheria dhidi yao.
"Sisi Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza hatuwezi kuacha kuwashughulikia ndiyo maana mwaka huu tumekuwa na Operesheni zaidi ya nne za kuwasaka wahalifu kwa lengo la kuzuia mauaji ya watu" Amesema Mutafugwa
Naye afisa mhifadhi daraja la kwanza Mary Kadeshi wa kituo kidogo cha Mwanza (TAWA) pamoja na kutoa elimu kuhusu nyara za Serikali, pia amesema Serikali inatambua uwepo wa waganga wa tiba asilia ambao wapo kisheria hivyo imeandaa utaratibu na ifikapo januari 2025 watu wataanza kuuziwa nyara ambazo zitakuwa halali kwa mmiliki atakae nunua na kupewa kibali kutoka Serikalini.
*Kutoka Dawati la Habari Polisi Mwanza*