Na Ghati Msamba.
Wakinamama wa Jimbo la Chalinze wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuleta nishati safi, baada ya kupokea majiko ya gesi 118 yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ndg. Ridhiwani Kikwete, kwa mama lishe wa kata 15 za jimbo hilo. Taarifa hii ilitolewa katika hafla iliyoandaliwa katika ofisi ya Mbunge huyo, ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria.
Katika hotuba yake, Ndg. Ridhiwani Kikwete alisema kuwa lengo kuu la kugawa majiko haya ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kudumisha mazingira bora na kuhamasisha matumizi ya nishati safi, hasa kwa wanawake wajasiriamali ambao kwa kawaida hutumia kuni na mkaa kupikia.
"Sasa mtakwenda kupika chakula kwa haraka na kwa usafi. Hii itasaidia kuboresha shughuli zenu na kuendelea kuunga mkono kampeni ya Rais Samia ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi," alisema Kikwete.
Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Dawati la Jinsia wa Halmashauri ya Chalinze, Bi. Recho Mnguruta, alieleza kuwa majiko hayo yatasaidia wanawake wajasiriamali kuondokana na madhara ya matumizi ya mkaa na kuni, ambayo ni hatari kwa afya na mazingira.
Naye Bi. Lilian Skawa, mkazi wa Msata, alieleza furaha yake kwa kupokea majiko hayo, akisema kuwa yamekuwa msaada mkubwa katika kazi zao za kila siku. Alisema kuwa kabla ya majiko ya gesi, walikuwa wanakutana na changamoto ya kupata mkaa hasa wakati wa mvua, ambapo mkaa ulikuwa unalowa na kuathiri ubora wa chakula.
"Kabla ya majiko haya, tulikuwa na changamoto kubwa ya mkaa, lakini sasa tutakuwa na mabadiliko makubwa. Tutapika kwa haraka na kwa usafi, na wateja wetu watapata chakula cha moto muda wote," alisema Bi. Skawa.