Ukosefu wa Ujuzi Miongoni mwa baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu pamoja na vya kati nchini umetajwa kuwa kikwazo kwa baadhi yao katika kupata ajira kwenye sekta binafsi.
Hatua hiyo inafuatia baadhi ya waajiri kutotoa nafasi za ajira baada ya kubaini kuwa baadhi ya wahitimu hawana ujuzi unaohitajika katika kuwawezesha kuongeza tija kwenye shughuli zao za uzalishaji mali.
Hayo yamebainishwa Jijini mwanza na Mshauri Mtaalam wa masuala ya ujengaji ujuzi kwa vijana kwenye Mradi wa Inclucities Thomas Aikaruwa wakati wa kikao baina ya baadhi ya waajiri pamoja na vyuo vinavyotoa mafunzo ya ujuzi na ufundi stadi mkoani mwanza kilicholenga kutafuta suluhisho la tatizo la ukosefu wa ujuzi miongoni mwa wahitimu wa fani mbalimbali.
‘’Kuna vijana wengi tunao mtaani ambao wanatafuta ajira lakini pia tunao waajiri wanaotafuta vijana wenye ujuzi unaohitajika kwenye maeneo yao ya kazi,kwa hiyo kumekuwa na pengo hilo kati ya waajiri na waajiriwa,kwa hiyo tumeamua kuwakutanisha pande zote mbili ili waweze kuzungumza pamoja na kuelewana nini hasa kifanyike kutatua tatizo hilo,Kwa Maana ya kwamba Waajiri waseme changamoto ninini wanapokuwa wanakutana na hawa vijana na wafundishaji nao waweze kusema nini hasa wanachokifanya kwenye mafunzo yao,wanapata changamoto gani kuwapa vijana ujuzi unaohitajika sokoni’’alisema Aikaruwa
Aikaruwa amesema kuwa Mradi wa Inclucities umebuniwa ili kuangalia namna ya kutatua tatizo la ujuzi miongoni mwa wahitimu wa vyuo na hatimaye kuliwezesha Taifa kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaohitajika kwenye soko.
Akizungumza kwenye kikao hicho,Katibu wa chama cha wafanyabiashara,wenye viwanda na kilimo(Tccia)Mkoa wa Mwanza Hassan Karambi amekiri kuwepo kwa changamoto ya ujuzi miongoni mwa baadhi ya wahitimu.
Karambi amesema kuwa kati ya vijana kumi hadi 15 wanaoingia kwenye soko la ajira ni watatu pekee ndio wenye ujuzi unaohitajika kwenye Sekta binafsi na hivyo kuchangia vijana wengi wanaotoka vyuoni kukosa fursa za ajira.
Naye Mkufunzi kutoka wakala wa elimu na mafunzo ya uvuvi(Feta)Kituo cha Mwanza Peter Masumbuko amesema kuwa wakala huo umebaini kuwa Mafunzo yanayotolewa na Wakala huo hayakidhi mahitaji ya soko la ajira.
‘’Na hiyo tumepata kutoka kwa waajiri wenyewe kwa maana ya sekta binafsi,kwa hiyo kupitia kikao hiki tumejifunza mengi ambapo tutatakiwa sasa kupitia upya mitaala yetu lakini pia kutengeneza platform ambayo itatuunganisha na hii sekta binafsi ili tuzalishe wahitimu wenye ujuzi wanaouhitaji’’alisema Masumbuko.
Kwa upande wake,Meneja wa shirika la kuhudumia viwanda vidogo nchini(Sido)Mkoa wa Mwanza Bakari Songwe amesema kuwa shirika hilo katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ujuzi miongoni mwa baadhi ya wahitimu limekuwa likiwapa mafunzo kwa vitendo pamoja na kuwaunganisha na wadau mbalimbali.
Mradi wa Inclucities unatekelezwa nchini kwenye miji ya Mwanza,Tanga na Pemba ambapo unalenga kukuza miji safi kwa kuwezesha biashara za uchumi kijani na rejeshi.