Ameyasema hayo MNEC Hamoud*akiwa katika Shina namba 13 Tawi la Inyanga Kata ya Mungula Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga, leo
"Tunapita kujenga umoja na mshikamano wa wanachama na viongozi kwa kufika katika ngazi za matawi na shina ili kukagua na kuimarisha uhai wa chama kuanzia ngazi ya mabalozi ambao ndiyo msingi mkubwa wa chama cha mapinduzi" alisema MNEC Hamoud
Miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele katika ziara hiyo ni suala la uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ambao unatarajia kufanyika mwezi ujao ambapo ametumia mikutano hiyo kuhamasisha wananchi na wanachama kujitokeza katika maboresho ya daftari la mkazi ili kuwa na haki ya kushiriki katika uchaguzi ujao,
Alisema Chama Cha Mapinduzi kinaamini katika Haki na usawa ambapo kimeandaa wagombea makini ambao wanaweza kukipa ushindi chama ili kiendelee kushika dola kama ilivyo katika malengo ya chama chochote cha siasa ya kushika dola.
Alisema viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wanapaswa kuendeleza umoja na ushirikiano baina yao ili kushinda katika chaguzi hizo badala ya kugawanyika na kuunda makundi yanaweza kukigawa chama na kusababisha mgawanyiko wa kura na kusababisha wapinzani kupita katikati kwa kushinda kitendo ambacho kitapelekea chama kushindwa.
"Malizeni makundi, migawanyiko na vurugu kati yenu, hatuwezi kushinda uchaguzi tukiwa hatujui tunataka nini, tunapokwenda kwenye uchaguzi tuwe wamoja" alisema
Tutende haki katika kuteua wagombea ili kupata kibali kwa wananchi kwani watu ni wengi wenye sifa wanaoweza kushinda na kukipa ushindi chama cha mapinduzi kutokana na kuwa chama chetu kinahazina kubwa ya viongozi.
"Tuteue viongozi wazuri wanaokubalika na wananchi hata tukiwapeleka huko wananchi waseme mtu huyu ndiye tuliye mtaka badala ya kubeba wagombea mfukoni, tunazo taarifa za baadhi ya viongozi waliowaweka mfukoni wagombea hiyo ni dhambi kubwa na haikubaliki"alisema Hamoud
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mungula, Skolastika Bebete, anaeleza namna miradi ilivyotekelezwa katika sekta mbalimbali ambapo serikali imetoa fedha kwaajili ya ujenzi wa shule na madarasa kwa ajili ya kuwawezesha wananchi,
"Tunaishukuru sana serikali kwa kutuwezesha utekelezaji wa miradi mingi kwenye kata yetu ambayo imewezesha upatikanaji wa maji kwenye kata yetu kuwa zaidi ya asilimia 85, umeme ni zaidi ya asilimia 75, imetupa fedha milioni 189 kwa ajili ya shule ya sekondari Inyanga Milioni 380 kwaajili ya shule ya msingi Mungula B,huku kwenye barabara serikali ikitoa milion 330.6 ili kukatavati miundombinu ya barabara lakini pia serikali ikitoa shilingi milioni 7.3 kwa ajili ya ukarabati wa zahanati ili kuimarisha afya za wananchi"alisema Bebete.