Na Mwandishi Wetu;NIRC
Wadau wa lishe nchini wameombwa kushirikiana na serikali katika kukabiliana na changamoto ya udumavu katika mkoa wa kagera.
Mkuu wa wilaya Muleba Dkt.Abel Nyamahanga ametoa wito huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo wakati akifungua maonesho ya wiki ya chakula duniani yanayoendelea Mkoani kagera kufuatia mkoa huo kukabiliwa na ongezeko la tatizo la udumavu.
Miongoni mwa wadau wanaoshiriki maonesho hayo ni pamoja na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.
Akizungumza kwenye maonesho hayo,Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uendeshaji kutoka Tume hiyo Salome Njau amesema kuwa Tume imejiandaa kutoa elimu ya kutosha kwa wakulima kuhusu namna bora ya uzalishaji na majukumu ya tume ikiwemo kusimamia,kuratibu na kuendeleza miundombinu yote ya umwagiliaji nchini.
Salome pia amewataka wakulima mkoani Kagera na maeneo jirani kutumia fursa ya maonesho hayo kunufaika na uwezeshaji unaofanywa na Tume kuhusu kilimo cha umwagiliaji ili kutimiza azma ya serikali ya kufikia kilimo cha kisasa na chenye tija kwa maslahi ya ndani pamoja na nje ya nchi ikiwemo kuilisha dunia.