Waziri wa viwanda na biashara Dkt. Seleman Jafo amesema kuwa serikali imeendelea kuondoa vikwazo kadhaa vya kibiashara ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa vibali ili kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizindua maonesho ya 19 ya biashara ya afrika mashariki yanayofanyika kwenye viwanja wa Furahisha Jijini Mwanza Jafo amewahasa wawekezaji kutumia fursa ya uwepo wa mazingira mazuri kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo viwanda na kilimo.
Amesema kuwa ongezeko la uwekezaji nchini ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa Uchumi,kuongeza nafasi za ajira Pamoja na kuongeza pato la Taifa
Aidha amezitaka halmashauri nchini kutenga maeneo ya uwekezaji Pamoja na Maeneo maalum ya maonesho ya kibiashara ili kurahisisha upatikanaji wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
Maonesho hayo yameandaliwa na chama cha wafanyabiashara,wenye viwanda na kilimo(TCCIA)Mkoa wa Mwanza ambapo pia waziri Jafo amekitaka chama hicho kuandaa maonesho hayo katika ngazi ya Taifa.
Naye mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Mwanza Gabriel Kenene ameiomba serikali kuondoa na kupunguza utitiri wa tozo zisizokuwa na msingi ambazo zinachangia wafanyabiashara wengi kutorasimisha biashara zao na kufanya biashara nje ya mfumo rasmi na hivyo kuikosesha serikali mapato.
Kenene amesema kuwa washiriki kutoka ndani na nje ya nchi watanufaika na ujuzi wa utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo za chakulakutoka kwa wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa kutoka mataifa bingwa wa teknolojia ikiwemo China na India
Maonesho hayo yatakayofikia tamati Septemba 15 mwaka huu yanazishirikisha zaidi ya makampuni mia mbili ya kibiashara kutoka ndani na nje ya nchi.