Na Shomari Binda-Musoma
WANAWAKE mkoa wa Mara wametakiwa kujitokeza kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la mpiga Kura kwa ajili kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Kauli hiyo imetolewa Leo Septemba 6, 2024 na Mjumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wanawake wa ( UWT) Taifa Rhobi Samwelly alipokuwa akizungumza na George Marato TV.
Amesema siku zote wanawake wamekuwa mstari wa mbele kwenye masuala mbalimbali yakiwemo ya uchaguzi.
Rhobi amesema katika zoezi hili la uboreshaji wa daftari kwa mkoa wa Mara lililoanza septemba 4 hadi 10 wanawake wote wenye sifa wanapaswa kujitokeza kushiriki zoezi hilo.
Mjumbe huyo wa baraza la UWT Taifa amesema wanawake wasisubiri hadi siku ya mwisho bali wajitokeze sasa kujiandikisha na kuboresha taarifa.
Amesema bila kujiandikisha na kuboresha taarifa huwezi kushiriki kikamilifu zoezi la uchaguzi pale litakapofika.
" Zimebaki takribani siku chache kuhitimisha zoezi la uboreshaji daftari la wapiga kura kwenye mkoa wetu lililoanza septemba 4.
Niwaombe wanawake na wananchi kwa ujumla kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa kwaajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025", amesema.
Rhobi amesema licha ya kujiandikisha na kuboresha taarifa wanapaswa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali zikiwemo za kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadae mwaka huu.