Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyakagwe Kata ya Butobela Wilaya ya Geita Daudi Lumala amekanusha vikali taarifa za uongo zinazosema kwamba wachimbaji wadogo wamekuwa wakidhulumiwa na matajiri katika machimbo yasiyo rasmi (rash) eneo la Mabunduki.
Kwa mujibu wa Lumala, uchimbaji katika eneo hilo unaendelea kwa amani na hakuna malalamiko yoyote kuhusu kuibiwa au kudhulumiwa dhahabu wakati wa kugawana wanapo zalisha dhahabu.
Ameeleza kuwa taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii hasa kwenye makundi sogozi(Whatsapp groups) ni taarifa za uongo na uzushi Maana hakuna mtu yeyote aliyedhulumiwa kwenye uzalishaji ambao umeisha fanyika katika machimbo hayo.
Mwenyekiti Lumala amesema kuwa katika uzalishaji wa hivi karibuni kimefanikiwa kusanya milioni 63 kutoka Mabunduki, ambazo zitajenga jengo la utawala katika shule ya sekondari Nyakagwe, ambapo walimu sasa wanatumia darasa kama ofisi.
Meneja wa rashi ya Mabunduki Mgusa Sylvester amesema kuwa uzalishaji uliopatikana umegawanywa bila malalamiko, na walilipa kodi za serikali na kutoa mchango wa maendeleo kijijini.