Serikali inakusudia kuboresha miundombinu ya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi iliyoko wilayani Ilemela Mkoani Mwanza ili kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia
Naibu waziri wa Maliasili na Utalii DUSTAN KITANDULA amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha,Serikali imetenga shilingi millioni Mia tano kwa ajili ya kuanza maboresho hayo ikiwemo kuanza ujenzi wa miundombinu mipya ya utoaji wa elimu.
KITANDULA amebainisha hayo wakati wa Mahafali ya 59 ya Taasisi hiyo baada ya kuelezwa kuhusu changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba pamoja na uchakavu wa baadhi ya miundombinu ikiwemo Mabweni,Madarasa na nyumba za watumishi.
Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi pia inakabiliwa na uhaba wa vifaa vya kisasa vya mafunzo ikiwemo GPS, Darubini,Radio calls na Silaha pamoja na uhaba wa magari ya kisasa Kwa ajili ya Mafunzo yakiwemo ya Waongoza Watalii.
Mkuu wa Taasisi hiyo Jeremiah Msigwa amesema kuwa changamoto hizo zinachangia katika kupunguza ufanisi wa utoaji wa elimu Bora.
Kuhusu changamoto ya ajira kwa kada ya askari wa uhifadhi,Naibu waziri wa Maliasili na Utalii DUSTAN KITANDULA amesisitiza dhamira ya serikali ya kuendelea kutoa nafasi za ajira kwa kada hiyo ili kukabiliana na uhitaji mkubwa wa Wataalam hao.
KITANDULA amewaasa wadau Wanaojihusisha na uhifadhi wa Wanyamapori na biashara zinazoendana na uhifadhi wa Wanyamapori kutoa nafasi za ajira kwa vijana ili kuongeza tija pamoja na kupunguza changamoto ya Ajira.
Katika kuongeza wigo wa ajira kwa wahitimu na kukuza mapato,Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi imeanzisha kampuni ya Ulinzi inayojulikana kwa Jina la Pasiansi Wildlife Security Company Ltd(PASCO) ambayo tayari imetoa ajira zaidi ya elfu nne kwa wahitimu ambao hawajapata ajira rasmi.