Wanawake wilayani misungwi mkoani mwanza wametakiwa kuacha kukopa fedha kwenye taasisi zisizo rasmi ili kuepuka kuingia kwenye migogoro wakati wa kurejesha mikopo hiyo.
Akizindua Jukwaa la uwezeshaji wa wanawake kiuchumi,Mkuu wa wilaya hiyo Johari Samizi amesema kuwa mikopo inayotolewa na Taasisi zisizo rasmi imekuwa ikiwaumiza wananchi kutokana na riba kubwa inayowekwa na wakopeshaji ambao hawazingatii taratibu za mikopo.
“Kuna Taasisi rasmi za fedha,tuache kwenda kukopa mikopo kausha damu,kuna mikopo ina majina mpaka unaogopa,yaani ukisikia mkopo mpaka apetitle ya kula inaisha,kuna mkopo unaitwa ngumu kumeza,Jina lenyewe linahataraisha usalama wako,mkopo kausha damu,damu ikikauka kuna uhai”alisema Samizi na kuongeza kuwa
“Mama zangu nawaomba sana,Mikopo hii inasambaratisha familia,ndoa zimevunjika na kuharibika kwa mahusiano,familia zinasambaratika kisa mkopo kausha damu,ndo maana nawaambia kopeni kwenye taasisi rasmi za kifedha,mkishindwa taasisi rasmi dirisha likifunguliwa nendeni halmashauri mkachukue mikopo ambayo haina riba”
Johari amewatahadharisha wanawake wa wilaya misungwi dhidi ya kuchukua mikopo na kutoweka kuwa serikali itakula nao sahani moja kuhakikisha kuwa wale wote wanaokopa wanarejesha fedha wanazokopa ili kuwezesha watu wengi zaidi kuweza kunufaika na fursa ya mikopo
Jukwaa hilo lenye kauli mbinu isemayo Kumuinua mwanamke kiuchumi kutana na fursa limelenga kuwaunganisha wanawake wa misungwi na fursa mbalimbali za kiuchumi pamoja na kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Katibu wa Jukwaa hilo Shamsa Mvamba amesema kauli mbiu hiyo inalenga kuhamasisha wanawake wote wa wilaya misungwi kujiunga kwenye vikundi vya uzalishaji mali ambavyo vitawawezesha kujipatia kipato njia ya kuwakutanisha na fursa mbalimbali zinazowazunguka.
Naye Mratibu wa dawati la uwezeshaji wananchi kiuchumi halmashauri ya wilaya misungwi Juliana Mwongereza amesema kuwa Jukwaa hilo litatumika kuwakutanisha wanawake na fursa mbalimbali za kiuchumi zikiwemo Mitaji na Mikopo.
“Jukwaa hili pia ni sehemu pekee ambayo wanawake wanaweza kuungana katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia,Maana inafika mahali watu wanaofanyiwa ukatili wanakosa mahali pa kwenda kusemea lakini kupitia Jukwaa watashirikiana na ofisi ya ustawi wa jamii na dawati la polisi la jinsia na watoto,lakini tuko nayo nyuma maendeleo ya jamii kuhakikisha tunapinga ukatili wa kijinsia”alisema Mwongereza
Kwa upande wake,Afisa wa polisi dawati la jinsia na watoto wilayani misungwi Mwanasa Mohamed amewaasa wanawake kujiepusha na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake.
“Tunapotafuta uchumi wa 50/50 haimaanishi umnyase mume wako,haimaanishi umnyanyase ule ubavu ambao ni wa kwako make wakati mnaanza naye alikusaidia kufikia hiyo 50/50,huu ni ukweli mchungu ni lazima tuelewe nafasi ya mwanaume katika familia,kuna leo,kuna uwezekano leo ukawa na kipato cha millioni moja lakini wakati mnaanza na mumeo ulikuwa huna uwezo wa kupata hata elfu kumi sasa hivi umefikia millioni moja yeye ana laki mbili bado endelea kumpa heshima yake kama mumeo”alisema Mwanasa