MFANYAKAZI WA PREMER CASKNO MWANZA AILILIA SERIKALI.
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MFANYAKAZI wa Premer Casino ya Mwanza katika Idara ya Ulinzi Bw Nassor Butondo amelalamikia kitendo cha kushambuliwa na wachina Agosti ak 30, mwaka huu, majira ya usiku wakati anatekeleza majukumu yake ya ulinzi, Jambo Digital imeelezwa.
Aidha Butondo ameulalamikia uongozi wa Casino hiyo iliyoko katika Jengo la Rock City Mall Wilayani Ilemela kwa kushindwa kumhudumia kimatibabu mlinzi wao huku wakitumia fedha nyingi kuwatibisha wachina walioanzisha fujo ndani ya Casino.
"Mwajili wangu anawathamini zaidi wachina kuliko mimi, ndio maana pengine ni kwasababu ndio wateja wa kamali, hivyo matusi yao ya nguoni inabidi wafanyakazi wayavumilie tu, wakati mwingine huwadhalilisha wafanyakazi wa kike kwa kuwaingizia vidole sehemu ambazo sio rasmi, Serikali itusaidie" alifafanua Butondo.
Imedaiwa kuwa siku hiyo kulitokea kutoelewana kati ya mchina na mzungu baada ya mchina (jina tunalo) kuliwa kwenye kamali na kuanzisha valangati ambapo Butondo alilazimika kufanya kazi yake ya kuzuia vurugu hizo.
Wakati akimzuia mchina huyo kumzonga zonga mzungu, wachina wengine zaidi ya 30 walinyanyuka na kuanza kumshambulia Butondo kwa kumpiga kwa viti katika sehemu mbalimbali za mwili na kumsababishia maumivu na majeraha makubwa.
"Wachina hao wameniumiza sana, maana kila walichoshika walinipiga nacho, walitumia viti vya humo Casino wakaniumiza sana angalia begani na mgongoni, naomba msaada kwa serikali" alilalamika Butondo.
Hata hivyo kuna madai kuwa mbali na Kamali inayochezwa ndani ya Casino hiyo lakini pia hufanyika biashara haramu ya kubadilisha na kukopesha pesa, biashara ambayo sio rasmi, kwa ujumla ni utakatishaji fedha ambao hufanywa na mchina mmojawapo.
Afisa utumishi wa Casino, James Lugendo alipozungumza na Jambo Digital ofisini kwake wiki iliyopita alikili kutokea kwa vurugu hizo lakini akadai yeye hakuwepo siku hiyo, bali alipata taarifa kutoka kwa mfanyakazi mwenzake kwa simu (hakumtaja) kuwa vurugu zimetokea ndani ya Casino.
"Sikuwepo lakini nilipigiwa simu nikiwa nyumbani nikaambiwa kuwa kumetokea ugomvi Casino, hata hivyo yalisuluhishwa yakaisha, kwa mfano wewe nyumbani kwako watoto wakigombania si unasuluhisha na baadae hali inatulia au sio?" alihoji Lugendo.
Hassan Masala ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama amezungumza kwa simu na Jambo Digital leo Septemba 8, 2024, akaahidi kufuatilia mambo yote yasiyo zingatia sheria ndani ya Casino hiyo.
"Nashukuru sana, ngoja tufuatilie taarifa hizo, na kama mambo hayo yapo ni makosa." alisema DC Masala.
Mwisho.