Na Emmanuel Chibasa
Katika jamii ya wakulima wadogo wadogo, matumizi ya kilimo cha umwagiliaji ni mbinu muhimu kwa ajili ya kukuza mazao ya mboga mboga na matunda. Hata hivyo, wakulima wengi wanakabiliwa na changamoto kutokana na mbinu wanazotumia. Kwa mfano, baadhi yao wanapanda mbegu moja kwa moja shambani, huku wengine wakipendelea kuotesha kwenye kitalu kabla ya kuhamishia miche shambani.
Kwa mujibu wa wizara ya kilimo, sekta ya kilimo kwa mwaka 2023 ilikua kwa asilimia 4.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.3 mwaka 2022 huku ikito ajira kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 65.6 na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda.
Licha ya uwepo wa hekta 727,280.6 za kilimo cha umwagiliaji na serikali kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima wadogo kuendesha shughuli zao za kilimo kwa kutumia wataalam pamoja na upatikanaji wa vifaa vya nishati ya umeme jua(solar) lakini bado wakulima wadogo wanakabiliwa na changamoto katika kilimo cha tija.
Mwandishi wa George Marato Tv amezungumza na baadhi ya wakulima wanaoendesha shughuli za kilimo katika kijiji cha nywatwali wilayani bunda mkoani Mara na kukukutana na Beatrice Nyamhokya ambaye ni mkulima wa mboga mboga anaendesha kilimo cha umwagiliaji na anatumia mbinu ya kuotesha mbegu kwenye kitalu kabla ya kuhamishia miche shambani.
Ingawa Beatrice anaendesha shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia pump za mafuta kumwagilia mazao yake, lakini anasema pump hiyo inatumiwa na wakulima wengine katika eneo hilo kaatika kumwagilia mazao yao.
Amesema kuotesha mbegu kwenye kitalu kunamwezesha kupata miche yenye afya na rutuba, ambayo ina uwezo mkubwa wa kustahimili magonjwa na wadudu pindi anapoihamishia shambani kwa ajili ya ukuaji. Anaeleza faida za mbinu hii ni pamoja na ongezeko la uzalishaji, mazao bora, na muda mdogo wa kupanda tena baada ya mavuno lakini changmoto kubwa anayokumbana nayo ni gharama za umwagiliaji kutokana na kutumia pump ya mafuta na pesa nyingi inatumika kununua mafuta.
"Kwa kutumia kitalu, naweza kudhibiti mazingira ya ukuaji wa miche yangu na kuhakikisha kuwa inakuwa na afya njema kabla ya kuhamishia shambani. Hii inasaidia kupata mavuno yenye ubora wa hali ya juu lakini changamoto ni umwagiliaji kwa kutumia pump ya mafuta na kila siku lazima tununue mafuta na kama hakuna hela ya mafuta basi tunanishindwa kumwagilia sababu hatuna njia mbadala hapa kumwagilia mazao yetu." Amesema Beatrice
Japhet Mwenura pia ni mkulima katika kijiji hicho anasema yeye uotesha mbegu moja kwa moja katika shamba lake na licha ya kutumia mfumo huo kwa moja shambani lakini amekuja kubaini kuna athari za kukumbana na magonjwa ya mimea na wadudu, pamoja na upungufu wa uzalishaji.
"Nimekuja kubaini kwamba ukipanda mbegu moja kwa moja shambani sio vizuri sababu nimekua nikirudia kupanda mbegu wakati wa parizi sababu mbegu nyingine zinakauka kutokana na kushambuliwa na magonjwa au kukauka na jua.
Ningependa kuwa na miche yenye afya bora, lakini kuto kupanda moja kwa moja mbegu shambani kunanifanya niwe na changamoto za udhibiti wa magonjwa na wadudu, na hivyo kushindwa kupata mavuno bora na hali duni ya maisha tunashindwa kumudu kununua solar ndio maana tunatumia pump za mafuta" Amesema Japhet
Beatrice Nyamhokya na Japhet Mwenura ni miongoni mwa wakulima wadogo wanaoendesha shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwa kulima mazao ya mboga mboga na matunda katika mkoa wa Mara ambao ukosefu wa elimu ya matumizi ya nishati jua(Solar) katika kupinguza gharama za uendeshaji pamoja na uoteshaji wa mbegu katika kitalu ili kupata miche yenye afya bado ni kikazo kikubwa katika kujikwamua kiuchumi.
Katika kuangazia changamoto za wakulima hawa nimezungumza na Marcelina Lubuva ambaye ni mtaalamu wa maswala ya kilimo kutoka ushirika wa wajasiliamali wa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine(SUGECO) Kilichopo mkoani Morogoro akizungumzia changamoto hiyo kwa wakulima anasema kupanda mbegu kwenye kitalu kabla ya kuhamishia shambani kunasaidia kuongeza uhai wa miche na kupunguza hatari ya magonjwa na ni muhimu kwa wakulima kumwagilia mazao yao mapema asubuhi, kabla jua halijapanda juu, ili kudumisha unyevunyevu wa udongo kwa muda mrefu na kupunguza hatari ya magonjwa na wadudu.
“ Ili kulima kilimo chenye tija kwanza mkulima anashauriwa kupanda mbegu kwenye kitalu kabla ya kupeleka shambani ili kuufanya mmea kukua kwa ustawi na kuepukana na kuathirika na wadudu wanao kula mimiea
Lakini pia katika kumwagilia inatakiwa mkulima amwagilie mazao yake asubuhi na jioni ili kuulinda mmea usiweze kuathirika na joto” Amesema Marcelina
Kwa upande wake Kastuli Morice Dalei ambaye ni mhandisi wa kilimo kutoka katika kutoka ushirika wa wajasiliamali wa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine(SUGECO) kilimo cha umwagiliaji katika mashamba ya wakulima kwa kutumia nishati ya umeme jua ni suluhisho la kuwaondolea gharama wakulima hasa wenye kipato cha chini.
Amesema matumizi ya nishati ya jua kwa umwagiliaji wa bustani unaweza kuwa suluhisho la gharama nafuu na endelevu. Mfumo wa umwagiliaji wa solar hutumia nishati ya jua kwa ajili ya kuendesha pampu za umwagiliaji, hivyo kupunguza matumizi ya nishati ya umeme na gharama za mafuta. Faida zake ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji, kupunguza athari za mazingira, na kuboresha upatikanaji wa maji katika maeneo yenye ukosefu wa umeme.
“Hapa SUGECO mwanzoni tulikua tunatumia umeme wa tanesco kumwagilia mazao na kisha tukanunua pump ya mafuta ambayo kwa siku tulikua tunatumia kuanzia lita ishirini ukipiga hesabu unakuta tunatumia gharama kubwa sana kuendesha shughuli hii lakni tangu tumefunga solar gharama za uendeshaji zimepungua sana, tunatumia solar muda wote na nawasihi wakulima watumie solar ili kupunguza gharama” Amesema Kastuli.
Mbinu ya kuotesha mbegu kwenye kitalu kabla ya kuhamishia shambani inabainika kuwa yenye manufaa zaidi kwa wakulima wadogo wadogo, ikilinganishwa na kupanda moja kwa moja shambani. Kwa ushauri wa wataalamu, wakulima wanaweza kuongeza tija na kuboresha mavuno yao kwa kutumia mbinu bora za umwagiliaji, kufuata muda sahihi wa kumwagilia, na kuzingatia matumizi ya nishati ya jua (solar) ili kuboresha hali ya kilimo na kupunguza gharama.
Licha ya takwimu kuonesha kuwa Tanzania bado inawatumiaji wachache wa wa matumizi ya nishati ya umeme jua Serikali kupitia wizara ya kilimo kwa mwaka 2023/2024 ilitenga shilingi bilioni 970.8 kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na tija, kuongeza ajira zenye staha na ushiriki wa vijana na wanawake katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na lishe, kuimarisha upatikanaji wa masoko, mitaji na mauzo na mazao nje ya nchi na kuimarisha maendeleo ya ushirika.