Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi ililipa fidia jumla ya Shilingi 2,576,081,789.00 kwa wananchi 142 waliopisha ujenzi wa barabara ya Kidatu - Ifakara (km 67) ,kwa Wananchi ambao nyumba zao zipo ndani ya hifadhi ya barabara ya mita 22.5.
Hayo yameelezwa leo Septemba 3,2024 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilombero Abubakar Asenga aliyeuliza Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopisha upanuzi wa barabara ya Kidatu kwenda Ifakara km 67.
"Zoezi la Ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara ya Kidatu - Ifakara (km 67) lilifanyika mwaka 2017 kwa kuzingatia Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007", amesema Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa kwa wananchi ambao nyumba zao zipo ndani ya hifadhi ya barabara ya mita 22.5 kutoka katikati ya barabara hawakustahili fidia kwa mujibu wa sheria.