PROFESA RIZIKI SHEMDOE ATAKA UVUVI HARAMU KUKOMESHWA ZIWA VICTORIA

GEORGE MARATO TV
0

Rai imetolewa kwa Mataifa ya Kenya, Uganda na Tanzania, kufanya doria ya pamoja katika ziwa victoria, ili kukomesha uvuvi haramu na biashara ya mazao ya uvuvi, inayokiuka taratibu za kisheria ndani ya ziwa hilo.

Akifungua mkutano leo Agosti 26,2024 wa kuhamasisha wadau wa uvuvi kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi ziwa victoria kwenye ukumbi wa mikutano Nyakahoja,Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof.Riziki Shemdoe amesema ziwa linamchango wa asilimia 67% katika sekta ya uvuvi nchini, likiwa limeshuka kwa asilimia 17% kutoka 85%, likiwa na wavuvi 100,002, huku wanufaika wa moja kwa moja wa biashara ya mazao ya uvuvi wakiwa zaidi ya laki mbili.

"Serikali kwa kutambua mchango wa sekta hii inaendelea kuiboresha ikiwa pamoja na kutoa boti za kisasa na ukopeshaji wa bila riba kwa makundi maalum wa Ufugaji wa samaki wa vizimba,lakini Pamoja na mchango huo, kikwazo kikubwa kinacholikabili ziwa hili ni uvuvi haramu unaoangamiza mazalia ya rasilimali zilizopo ziwani humo",amesisitiza Katibu Mkuu.

Amewataka wadau wa sekta ya uvuvi kukaa na kuja na mikakati endelevu ya kimataifa ya kukomesha hali hiyo na kuwasilisha Serikalini ili ifanyiwe maboresho mazuri na ziwa liendelee kuwa na tija kwa wananchi wa Mwanza na nchi jirani.


"Napenda kuchukua nafasi kuwafahamisha pia mradi wa uvuvi wa kutumia boti za kisasa umefanya vizuri tumetoa boti 160 nchi nzima na 151 zimefanya vizuri",Prof.Riziki Shemdoe

Kwa upande wake Mkurugenzi wa uvuvi kutoka Wizara ya mifugo na uvuvi Profesa Mohamed Sheikh, amesema hali ya uvuvi haramu imechangia uvunaji wa tani za samaki kushuka katika ziwa victoria, ukihusisha sangara, dagaa, mabondo na mauzo kuporomoka.

"Wizara inakuja na mkakati wa kisasa wa kupambana na hali hiyo ukiwemo utumiaji wa ndege nyuki ili kuwabaini wanaojihusisha na uvuvi haramu na vifaa maalum vya ufuatiliaji,"Prof.Sheikh

Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Uzalishaji,Bw. Emil Kasagara akitoa taarifa fupi kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza,amesema viwanda vingi kwa sasa vinashindwa kujiendesha kwa ufanisi na vingine vikiyumba kutokana na upungufu wa rasilimali hizo unaochangiwa na uvuvi haramu.

"Tumekuwa na vikao mbalimbali na wadau wa sekta hii kwa lengo la kuelimishana na kuhakikisha ziwa linaendelea kuwa kitega uchumi muhimu kwa wananchi",Kasagara.

Mkutano huo umewashirikisha Maafisa uvuvi kutoka Mwanza,mikoa ya jirani na sekta binafsi.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top