Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeendelea na jitihada za kuimarisha mifumo ya kiusalama na kutokomeza vitendo vya kihalifu katika fukwe, mialo na visiwa ndani ya Ziwa Viktoria kwa kuishirikisha Jamii.
Uzinduzi wa operesheni sambamba na utoaji wa elimu kwa wananchi umefanyika Agosti 20, 2024 katika mwalo wa Igombe, Kata ya Bugogwa Wilaya ya Ilemala mkoani humo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa.
Akizungumza na uongozi wa Serikali za Mitaa na wananchi wa kata hiyo baada ya kuwapatia elimu ya usalama majini na ukatili wa kijinsia kutoka kwa Mkuu wa Kikosi cha Wanamaji mkoa wa Mwanza Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Wenceslaus Muchunguzi,
Kamanda Mutafungwa amezindua awamu nyingine ya kusikiliza kero za kiusalama kutoka kwa wananchi.
"Katika eneo lenu hili, siku ya leo nimekuja kuzindua awamu nyingine ya kusikiliza kero, changamoto, malalamiko na kupata ushauri kutoka kwa wananchi" amesema Kamanda Mutafungwa.
Aidha, Kamanda Mutafungwa amewaasa wananchi wa kata ya Bugogwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kuzuia uhalifu kuanzia ngazi ya familia kwani jukumu la ulinzi na usalama ni jamii nzima.
Kwa upande wake, Juma Kavilondo amekiri kutokuwepo kwa uhalifu wa kutumia Silaha katika ziwa Viktoria na umekuwa historia kwani Jeshi la Polisi limeudhibiti kwa kiasi kikubwa.
"Ule ujambazi uliokuwa unafanyika wa Silaha sijauona kwa muda mrefu labda ni matukio baadhi tu ya udokozi" amesema Kavilondo
Pia, Thadeo Philip @Bonge amepongeza Jeshi la Polisi kwa kudhibiti uhalifu wa kutumia Silaha akilinganisha na kipindi cha nyuma.
"Tangia umekuja mkoa wa Mwanza Kamanda Mutafungwa hatujawahi kusikia Bunduki inalia Igombe naomba niseme tuu ukweli kama ulivyo " amedokeza Bonge.
Sambamba na kuendelea kutoa elimu ya Polisi Jamii katika makundi mbalimbali ya kijamii, Kamanda Mutafungwa pia amepita katika Soko la kimataifa la Samaki na Dagaa Mwoloni, Kirumba na kutangaza operesheni kali ya kuwasaka wahalifu katika maeneo yote yaliyopo pembezoni mwa ziwa Viktoria na visiwa vya mkoa wa Mwanza.