Na Jovina Massano; Musoma
MGOMBEA udiwani Kata ya Mwisenge jimbo la Musoma mjini mkoani Mara Alphonce Dismas Ochieng ameahidi kutatua changamoto zilizopo kwenye Kata ili kupunguza malalamiko kwa wananchi ameyasema hayo Septemba 28,2025 wakati akinadi sera zake mtaa wa Mkinyerero.
Alphonce amesema kumekuwepo na malalamiko mengi kwa jamii hii inatokana na kutokutatuliwa kwa changamoto zinazowakabili wananchi.
Amesema baadhi ya mitaa ya Kata hiyo inakabiliwa na changamoto za ukosefu wa miundombinu rafiki ya barabara hasa katika mtaa huo wa Mkinyerero.
"Endapo nitapata ridhaa ya kuwa diwani nitawaomba wakala wa barabara mijini na vijijini TARURA kuangalia namna wanavyoweza kutatua changamoto ya barabara hapa Mkinyerero", amesema Alphonce.
Aidha amewaambia wakazi hao kuwa wakimchagua atasaidia kuwezesha wahitaji wenye vigezo walengwa watakaohudumiwa na mfuko wa Kaya maskini (TASAF) tofauti na ilivyo sasa.
Amesema wazee wengi wanaachwa ambao wana maisha duni na wanawezeshwa wenye uwezo wa kufanya kazi walio na vipato.
Sanjari na hayo amewaeleza wakazi hao namna atakavyoishauri mamlaka kuwekeza katika Kata ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa Kata ma kuleta Maendeleo kwa jamii kwa kuitumia vema fukwe ya ziwa iliyopo kwenye Kata kwa kuweka boti za michezo kuvutia watalii.
Amewasihi wakazi hao kujitokeza kupiga kura Oktoba 29,2025 na kuchagua viongozi watakaowawakilisha vema na kutatua changamoto zilizopo.