Ufanisi wa Ukusanyaji Mapato Wailetea Tanzania Maendeleo

GEORGE MARATO TV
0


Na mwandishi wetu Jovina Massano.

UFANISI katika mapato ya kikodi nchini Tanzania kumewezesha uendelezaji wa miundombinu mbalimbali ukiwemo  ushiriki wa sekta binafsi Pamoja na uimarishaji wa masoko ya mitaji na dhamana inayotumika kufadhili miradi hiyo.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango wakati aliposhiriki majadiliano ya Viongozi wa Juu kuhusiana na Umuhimu wa kutumia Rasilimali za Bara la Afrika kwa ufanisi itakayopelekea  kuchochea Maendeleo.

 Majadiliano hayo yaliyofanyika wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika katika Hoteli ya Sofitel Ivoire Jijini Abidjan nchini Ivory Coast.

Amesema kutokana na umuhimu wa miundombinu katika mageuzi ya kiuchumi nchini Tanzania, Serikali ilihitaji kufanya kazi zaidi katika kukusanya fedha ya uendelezaji wa miundombinu ikiwemo Reli ya kisasa (SGR) pamoja na barabara kuu ambazo zitaunganisha mataifa mbalimbali na kuwezesha ufanyaji biashara.

Makamu wa Rais ametaja juhudi za serikali katika ukusanyaji mapato ya ndani na kufadhili miradi ikiwemo kuimarisha usimamizi wa kodi kama vile ukusanyaji kupitia mifumo ya kielektoniki, kuwepo kwa Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko ya walipa kodi ili kuwawezesha walipa kodi kuweza kutoa changamoto zao pamoja na kukuza wigo wa soko la mitaji na dhamana kama vile uwepo wa hatifungani mbalimbali.

Hatua zingine ambazo Tanzania imepitia katika kuimarisha miundombinu ni pamoja na matumizi ya mifuko ya hifadhi ya jamii katika ujenzi wa barabara na madaraja pamoja na kutumia vema mikopo nafuu kutoka mashirika ya fedha kimataifa na nchi marafiki.

Aidha Makamu wa Rais ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na Rais wa AfDB anayemaliza muda wake Dkt. Akinumwi Adesina kwa kushirikiana vema na Tanzania katika kipindi cha uongozi wake ikiwemo kuwezesha ujenzi wa barabara, uwanja wa ndege pamoja na reli ya kisasa (SGR) kuelekea nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo.

Ameeleza kuwa Tanzania imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya nishati kwa lengo la kuharakisha maendeleo ikiwemo uwekezaji mkubwa katika mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao umekamilika na unazalisha megawati 2115.

Pia uwekezaji katika miradi mingine ikiwemo matumizi ya gesi asilia pamoja kuanza uzalishaji wa nishati ya joto ardhi ambayo itaanza kwa kuzalisha megawati 500.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top