Serikali imetangaza nyongeza ya mshahara kwa asilimia 35.1 kwa wafanyakazi wanaolipwa kima cha chini cha mshahara nchini kutoka 370,000 hadi 500,000.
Ameyasema hayo Rais Samia Suluhu Hassan Mei 1, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika katika Uwanja wa Bombardier, mkoani Singida.
Aidha, Rais Samia amesema serikali imepokea ombi la wafanyakazi wa umma kuhusu kutotumika kwa posho katika makato ya kodi, na kuahidi kulifikisha suala hilo kwa vyombo husika vinavyoshughulikia masuala ya mapato.
"Serikali inatambua mchango wenu na itaendelea kuboresha maslahi yenu kadri hali ya uchumi inavyoruhusu," amesema Rais Samia.