Na Shomari Binda-Musoma
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) Dkt.Emanuel Nchimbi amesema wanaotaka nafasi ya ubunge na kuwachafua walioko madarakani hawatapita kwenye mikono yake.
Kauli hiyo ameitoa leo aprili 23 kwenye ukumbi wa mikutano wa CCM mkoa alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho kwenye kikao cha ndani.
Amesema ni jambo la ajabu kuona wana CCM wanaandaa vijana kuwachafua na kuwazomea wabunge walioko madarakani na kudai kufanya hivyo ni kukichafua chama hicho.
Dkt.Nchimbi amesema kamwe hawataweza kuwavumilia wanachama wanaofanya vitendo hivyo kwa kuwa ni utovu mkubwa wa nidhamu.
Amesema yoyote atakayebainika kwenye vikao atakavyoshiriki yeye vya uteuzi halitapita jina la mwanachama huyo hata kama atashinda kwa kura nyingi.
" Ipo tabia mbaya ambayo imeibuka ya kuwachafua wabunge waliopo madarakani hili halikubaliki na hatua zitachukuliwa kwa wanaofanya hivi.
" Unapo mchafua mbunge kuwa hajafanya kitu ni kwamba unasema Chama hakijafanya kitu tusichafuane tunapoelekea kwenye uchaguzi",amesema.
Mbunge wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo amesema utekelezaji kwenye jimbo la Musoma mjini umetekelezwa vyema kwenye miradi mbalimbali.
Amesema kinachopiganiwa kwa sasa ni wananchi kuwa na uchumi na kumuomba Katibu Mkuu kusukuma suala la kufunguliwa kwa viwanda.
Mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo amesema jimbo pekee ambalo litatoa ushindi mapema kwa chama cha Mapinduzi ni jimbo hilo.
Amesema ujenzi wa shule zikiwemo za " High Schools unaendelea kwa kasi na kuomba kutiwa msukumo wa uanzishwaji wa viwanda vipya vikiwemo vya samaki kwenye jimbo hilo.