Na MASHAKA MHANDO, Pangani
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Zubeir Ali Maulid, amewataka Watanzania wauenzi na kuulinza Muungano kwa kushiriki uchaguzi Mkuu ujao kwa kuchagua viongozi sahihi.
Akizungumza Leo April 25 baada ya kukagua na kuzindua madarasa sita ya shule ya sekondari ya Bushiri wilayani hapa, alisema Muungano ni tunu iliyoasisiwa na viongozi hivyo hakuna budi kuulinda kwa nguvu zote.
Alisema Watanzania wanapoazimisha miaka 61 ya Muungano, wanatakiwa kukumbuka faida na fursa zilizotokana na Muungano huo lakini pia kutazama namna ya kuepuka chokochoko zenye viashiria vya kuvunja Muungano huo.
"Wote hapa zaidi ya asilimia 80 tuliopo hapa tumezaliwa ndani ya Muungano hivyo tunayo sababu kubwa ya kuenzi, kuulinda kwa kushiriki uchaguzi Mkuu ujao ili tuwapate viongozi wetu," alisema na kuongeza,
"Tunapoadhimisha maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wetu tunatakiwa tukumbuke faida na fursa zilizopatikana kupitia Muungano wetu,".
Akizungumza kuhusu shule ya Bushiri ambayo aliridhishwa na ujenzi wake, alisema ujenzi wa madarasa hayo uendane na ufaulu wa wanafunzi.
Alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuwaletea maendeleo wananchi katika sekta mbalimbali za kijamii.
Awali Ofisa elimu sekondari wa wilaya Pangani Lucy Gurtu alisema madarasa hayo yaliyogharimu shilingi milioni 116 yatatumiwa na wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
Mkuu wa wilaya ya Pangani Gift Msuya alisema kuwa Rais Dkt Samia Suluhu kwa kipindi chake cha miaka minne ameleta kiasi cha sh. 39,101,185,696.78 kwa miradi yote ya maendeleo na fedha za utawala.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na mbunge wa Mkinga, Dastan Kitandula ambaye serikali imempa jukumu la kuambatana na spika huyo alisema kuwa ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM katika mkoa wa Tanga imetekeleza kwa kiwango kikubwa ambacho shukrani za wananchi wa Tanga kwa Rais ni kumpa kura za kishindo uchaguzi ujao.
Kaimu Mkuu wa mkoa wa Tanga na Mkuu wa wilaya ya Mkinga, Gilbert Kalima alisema Spika wa BWZ anafanya ziara mkoani Tanga kwa kukagua miradi ya maendeleo katika wilaya za Tanga, Handeni, Pangani, Mkinga na Muheza.
Alisema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika mkoa wa Tanga ameleta jumla ya shilingi Trillion 1.3 zilizotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.
Katibu wa CCM mkoani Tanga Mfaume Kizigho alimpongeza spika huyo kwamba somo alilotoa kuhusu Muungano ni Elimu kubwa ameiacha katika mkoa wa Tanga na kwamba watu watakuwa wamejifunza na kuelewa.