MASHAKA MHANDO, Tanga
MKUU wa mkoa wa Tanga, Balozi Dkt Batlida Burian ameiagiza halmashauri ya Jiji la Tanga, kuharakisha ukarabati wa soko la Ngamiani ili mvua zinazoendelea kunyesha zisiharibu bidhaa za wafanyabiashara.
Akizungumza katika soko hilo jana, alipofika kukagua na kuona shughuli za wafanyabiashara hao, Dkt Batlida pia aliagiza mkandarasi anayekarabati soko hilo awe na wafanyakazi wa kutosha ili kazi hiyo isichukue muda mrefu.
"Mkurugenzi hakikisheni kazi ya ukarabati inakwenda kwa haraka, mnajua kipindi hiki ni cha mvua lazima tulinde bidhaa za wafanyabiashara wetu, hakikisheni mnakuwa na wafanyakazi wa kutosha ikibidi tunaweza kuongeza wafungwa ili soko likamilike kwa haraka," alisema Mkuu wa mkoa.
Mkuu wa mkoa aliwataka wafanyabiashara wawe watulivu katika kipindi hiki cha matengenezo na kwakuwa soko linakarabatiwa huku wakiendelea kuuza bidhaa zao basi wasiwe kikwazo kwa wafanyakazi wa mkandarasi.
Alimwagiza Mkurugenzi pia kuhakikisha wafanyabiashara wa soko hilo wanapata upendeleo wa mikopo ili waweze kuongeza mitaji yao hasa akina mama waliopo sokoni hapo.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Tanga, Rusajo Gwakisa alisema halmashauri ya Jiji hilo imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 na watakarabati soko hilo kwa awamu.
Alisema awali kazi ya ukarabati wa soko hilo ulikuwa uanze mapema mwezi uliopita lakini wafanyabiasha waliomba mkandarasi asubiri hadi kumalizika kwa kipindi cha mwezi wa Ramadhani na Kwarezima.
Soko hilo lililoanzoshwa mwaka 1951 linakarabatiwa na mkandari wa kampuni ya M/S Spacettec ya Jiji ya Arusha na mkataba wake ni wa siku 90.