Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania JWTZ limesema zoezi la pamoja la ‘AIKEYME’ limekuwa na mafanikio makubwa katika kupambana na changamoto mbalimbali za Bahari hasa katika ukanda wa bahari ya hindi.
Hayo yamebainishwa Aprili 18 Mwaka 2025 na Meja Jenerali Marco Elisha Gaguti ,wakati akizungumza kwenye hafla fupi ya ufungaji wa zoezi la pamoja la ulinzi wa Bahari maarufu kama ‘AIKEYME’ alipomwakilisha Mkuu wa Majeshi nchini Jenenerali Jacob John Mkunda, katika zoezi lililoandaliwa na Tanzania na India huku likishilikisha mataifa mengine tisa.
Aidha, Meja Jenerali Gaguti amempongeza Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Ulinzi wa nchini India kwa kuandaa zoezi hilo na huku akisema kuwa lengo kuu la zoezi hilo la pamoja ‘AIKEYME’ ni kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto baharini na kubadirishana uzoefu pamoja na kutengeneza mfumo wa kusaidiana katika ukanda wa Bahari ya hindi.
Hata hivyo, Meja jenerali Gaguti amesema kuwa kwa niaba ya mkuu wa majeshi nchini matumaini yake ni kuona zoezi hio la pamoja litaufanya ukanda wa bahari ya hindi kuwa salama na kupelekea kukomesha shughuli mbalimbali haramu katika ukanda huwo.
Kwa Upande wake Mwambata Jeshi la India nchini Tanzania Commodore Agyapal Singh amemshukuru Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Lawrence Tax na Mkuu wa majeshi nchini Jenerali Jacob John Mkunda kwa kufanikisha kufanyika zoezi hilo hapa nchini.
Kufanikiwa kwa kuhitimishwa kwa zoezi la pamoja maarufu kama AIKEYME kutasaidia kutokomeza na kukomesha shughuli mbalimbali harama za magendo katika ukanda wa Bahari ya hindi kupitia mazoezi mbalimbali ya utayari yaliyofanyika katika kuboresha uimara na kuimarisha uhodari wa askari katika kutimiza majukumu mbalimbali nchini.