Katika kikao hicho, viongozi hao walijadili kwa kina namna mbalimbali za kupunguza gharama za miamala ya kifedha, kudhibiti uhalifu wa kimtandao, na kuimarisha utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi. Masuala hayo yanalenga kupunguza matumizi ya fedha taslimu pamoja na kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma rasmi za kifedha, hasa zile zinazotolewa kwa njia ya kidigitali.
Aidha, kampuni ya VISA ilieleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania kwa kutoa mafunzo na kubadilishana ujuzi wa kitaalamu, ili kuimarisha mifumo ya malipo kuwa salama, rahisi na jumuishi kwa Watanzania wote.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Gavana, Dkt. Yamungu Kayandabila, Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi BoT, Dkt. Suleiman Missango, Meneja wa Sera ya Fedha BoT, Bi. Asimwe Bashagi, pamoja na maafisa waandamizi kutoka kampuni ya VISA.
Mazungumzo hayo yamefanyika sambamba na Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya IMF na Benki ya Dunia, inayoendelea jijini Washington D.C., Marekani.