Ujenzi wa vivuko vipya vitano unaotekelezwa na serikali kwa zaidi ya shilingi billion 50 unatarajia kuimarisha usafiri wa majini katika ziwa victoria.
Vivuko hivyo vinavyojengwa na mkandarasi wa kampuni ya kizalendo ya Songoro marine ya Jijini Mwanza ni Bwiro-Bukondo,Rugezi-Kisorya,Nyakaliro-Kome,Ijinga-Kahangara pamoja na Buyagu Mbarika
Waziri wa ujenzi Abdalah Ulega amekagua maendeleo ya ujenzi wa vivuko hivyo unaotekelezwa na serikali kupitia wakala wa ufundi na umeme(Temesa)na kueleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa.
Waziri Ulega amesema kuwa vivuko vinne kati ya vitano vitaanza kutoa huduma ya usafiri wa majini kwenye ziwa victoria ifikapo mwezi April mwaka huu na kuwaondolea baadhi ya wananchi wa wilaya za Misungwi,Sengerema,Ukerewe,Bunda na Magu adha ya usafiri inayowakabili hivi sasa.
Aidha amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa vivuko ili kutatua adha ya usafiri kwenye baadhi ya visiwa vilivyoko kwenye ziwa victoria.
Naye mkurugenzi wa kampuni ya songoro marine Major Songoro akitoa Taarifa kwa waziri Ulega amesema kuwa ujenzi wa kivuko cha Bwiro-Bukondo kitakachokuwa na uwezo wa kubeba abiria mia mbili pamoja na Tani mia moja za mizigo umefikia asilimia 91.3 na kitakamilika ifikapo machi 31 mwaka huu.
‘’Kivuko cha Rugezi-Kisorya kimefikia asilimia 80.5 na kinatarajia kukamilika ifikapo machi 29 mwaka huu,Kivuko cha Nyakaliro-Kome kimefikia asilimia 83.19 na kinatarajiwa kukamilika machi 29 mwaka huu,kivuko cha Ijinga-Khangara kiko asilimia 90.7 na kitakamilika machi 31 mwaka huu huku Kivuko cha Tano cha Mbarika-Buyagu kikiwa asilimia 80.5 na kinatarajiwa kukamilika ifikapo Julai nne Mwaka huu’’alisema Songoro
Akizungumza wakati wa ziara hiyo,Mbunge wa Jimbo la Sengerema Hamisi Tabasamu amemshukuru Rais Samia kwa kuondoa kero ya usafiri inayowakabili wakazi wa mbarika wilayani misungwi na Buyagu wilayani Sengerema pamoja na baadhi ya maeneo ya wilaya Nyangh’wale Mkoani Geita
‘’Changamoto ya usafiri wa Majini kati ya eneo la Mbarika na Buyagu imedumu kwa zaidi ya miaka 50 tangu kuzama kwa kivuko kilichokuwa kikitoa huduma kwenye eneo hilo na sasa tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Samia kwa kuondoa adha ya usafiri katika eneo hilo’’alisema Tabasamu.








