Na Shomari Binda-Musoma
VIONGOZI wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) Kata ya Mwisenge wamemuomba mbunge wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo kugombea tena nafasi hiyo uchaguzi wa mwaka huu wa 2025.
Wakizungumza kwenye ofisi za Kata za chama hicho wamesema kazi zilizofanywa na mbunge huyo za maendeleo zinapaswa kuungwa mkono.
Akiongoza viongozi hao Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mwisenge Mnyugu amesema si vibaya kusema mazuri yaliyofanywa na mbunge na wao kama viongozi wa Kata wametangaza kumuunga mkono.
Mnyugu amesema amesema muda ukifika kwa utaratibu wa chama achukue fomu na wao wapo tayari kumuunga mkono.
Mwenyekiti huyo amesema iwapo mbunge huyo atachukua fomu na kushinda katika kura za maoni itakuwa ni rahisi kushinda kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
" Tumekutana hapa kama viongozi wa Kata kumuomba mbunge Vedastus Mathayo kugombea ubunge uchaguzi wa mwaka 2025 muda ukifika.
" Tunatoa msimamo huu kutokana na kazi alizozifanya kuanzia kwenye miradi ya elimu,afya,maji,barabara na kuwezesha vijana shughuli za kiuchumi",amesema.
Amesema hivi karibuni watafanya kikao kikubwa kwaajili ya kuchanga fedha kwaajili ya kumchangia na kumuwezesha mbunge huyo kuchukua fomu
Mmoja wa viongozi hao amesema kazi zilizofanywa kila mmoja anaziona na kwa kutambua kazi hizo wanamuunga mkono kwa moyo wa dhati.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa wa Kata hiyo Yusuf Mwangwa ambaye ni Katibu wa vijana ( UVCCM) Kata ya Mwisenge amesema hawana sababu za kutokwenda na Mathayo kwenye uchaguzi wa mwaka 2025
Aidha viongozi hao wamempongeza Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa na kupitishwa kuwa mgombea wa chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka 2025.