Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe Hamza Johari amesema tasnia ya sheria nchini imepata pigo kubwa kufuatia kifo cha mwanasheria mkuu wa Serikaki mstaafu na Jaji mstaafu wa mahakama kuu Frederick Mwita Werema.
Ametoa kauli hiyo katika kijiji cha Kongoto wilaya ya Butiama mkoani Mara,wakati wa mazishi Jaji Werema, yaliongozwa na Jaji mkuu wa Tanzania mh Prof Ibrahim Juma, januari 4-2025.
Akitoa salamu za Pole, Mwanasheria huyu Mkuu wa Serikali, amesema kuwa Jaji Werema alijitolea kwa hali na mali katika kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria na kwa uwazi.
Alipambana na changamoto nyingi zilizokuwa zikiikabili tasnia ya sheria na hakusita kuanzisha mabadiliko yaliyoleta matokeo chanya kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Huu ni urithi mkubwa ambao utaendelea kuwa mfano na msingi wa kazi yetu sote tunaoendelea nayo leo.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesisitiza kuienzi na kuiendeleza misingi na mifumo ya sheria aliyoianzisha Jaji Werema kwa ustawi wa sekta ya sheria na taifa kwa ujumla.
“Kazi yake ni nguzo ya msingi kwa maendeleo ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kwa maendeleo ya sekta ya sheria nchini kwa ujumla”. Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mhe. Johari amesema marehemu Jaji Werema, ameacha alama isiyofutika katika tasnia ya sheria na Utumishi wa Umma nchini, atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwa taifa katika masuala mbalimbali ya kisheria na utendaji wa haki.
Kwa upande wake Jaji mkuu katika salamu zake,amesema kuwa marehemu jaji Werema aliamini kuwa kazi ya uwakili ni huduma bora na ya heshima,hivyo inapaswa kufanywa kwa umakini na weledi mkubwa.
"Alikuwa akisema hakuna sababu ya kujiita wakili msomi wakati kazi zako sio za viwango,yeye alikuwa akijiamiji kwa viwango"alisema jaji mkuu.
Jaji mkuu amesema kuwa nafasi ya mwanasheria mkuu wa serikali ni nyeti na ambayo ina majukumu mengi yanapapaswa kufanyika kwa pamoja hivyo inahitaji mtu mwenye uwezo mkubwa.
Katika mazishi hayo ambayo yaliongozwa na kanisani katoliki jimbo la Musoma kwa kushirikisha mapadri watano wakiongzwa na paroko wa Musoma Mjini Padre Medady Chegere,wamehudhuriwa na maelfu ya wananchi wa kijiji cha Kongoto na maeneo jirani ya Tarafa ya Kiagata,viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya mkoa wa Mara.
Miongoni mwa viongozi hao wa Serikali na vyama vya siasa wakiwemo wastaafu ni pamoja na mwenyekiti wa taasisi ya Mwalimu Nyerere mzee Joseph Butiku,waziri wa ardhi mstaafu Anna Tibaijuka,katibu mkuu kiongozi mstaafu Phillip Luanjo,kaimu mkuu wa mkoa wa Mara,mkuu wa mkoa wa Mwanza Said Mtanda,mbunge wa jimbo la Butiama na naibu waziri wa katiba na sheria Mh Jumanne Sagini,mbunge wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo,Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara Patrick Chandi pamoja na Mzee wa mila wa koo ya Wakenye Christopher Gachuma.
Majaji wa mahakama ya rufani na mahakama mkuu walipamba mazishi hayo kwa gwaride wakati wa kuaga mwili pamoja na kushiriki katika taratibu zote eneo la kaburi.
Jaji Werema ambaye akizaliwa Oktoba 10 mwaka 1955 alifariki desemba 30 mwaka 2024 wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili,ameacha mjane na watoto watatu