Na Angela Sebastian Bukoba
Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka waandishi na vyombo vya habari kuandika habari kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu za uchaguzi tunapoelekea uchaguzi mkuu kwa ajili ya usalama wa Taifa letu na wananchi wake.
Mhandisi Kadaya Baluhye meneja wa kitengo cha watumiaji huduma masuala ya mawasiliano kutoka TCRA makao makuu ametoa ushauri huo wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Kagera, kutoka vyombo mbalimbali vya habari ambayo yamefanyika mjini Bukoba.
Mhandisi Baluhye amesema kuwa kufuata kanununi na sheria za uchaguzi zinampa mwandishi mwongozo wa namna ya kuandika au kuendesha vipindi kwa usahii na usalama.
"Mwaka kesho ni uchaguzi mkuu ambao unagusa uchaguzi wadiwani,wabunge na Rais kwa kushirikisha vyama mbalimbali hivyo tuwe makini kwa kufuata kanununi,sheria na taratibu za uchaguzi na kutopendelea na kuweka ushabiki wa vyama mbele ili kulinda usalama wetu na nchi yetu maana wapo baadhi yetu wanatumika na kujisahau kuwa zipo kanuni na sheria hivyo tuzisome na kuzielewa kabla ya kujiingiza matatani"ameeleza Baluhye
Kwa upande wa Mhandisi Imelda Salum meneja TCRA kanda ya ziwa pia amewataka waandishi na watangazaji kutoegemea upande wowote na kutumia vyanzo sahii wanapoandika habari na kuandaa ili kuepuka kujiingiza kwenye migogoro isiyo ya lazima.
Aidha amesema kuwa mamlaka hiyo ipo kwa ajili ya kuwawezesha waandishi wa habari,wadau na vyombo vya habari kutambua wanafanya nini wanapofanya kazi zao ili kujiepusha na madhara ambayo yanaweza kuwapata.
"Wakati ule mwandishi ulipokuwa ukiandika habari au kutangaza habari ambazo hazijafuata misingi ya taaluma chombo kilifungiwa lakini kwa taratibu za sasa anayewajibishwa ni mwandishi mwenyewe hivyo tunapoandika na kutangaza tufuate misingi ya kazi zetu ikiwemo usahihi na vyanzo sahii ambazo zinazozingatia maslahi ya Taifa na ustawi wa wananchi"ameeleza Imelda
Amesema waandishi kukosoa Serikali siyo vibaya lakini tusiegemee upande mmoja tuangalie ukosoaji huo una maslahi kwa Taifa na wananchi wetu na wewe mwenyewe unayeandika na kutangaza bila kuweka hisia zetu hii itatujenga na kutuweka katika nafasi nzuri.
Naye mhandisi kutoka kitengo cha leseni makao makuu TCRA Aule Kileo alisema mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na wadau na waandishi wa habari kuahakikisha wanatatua changamoto katika utoaji wa huduma ili kuleta tija inayokusudiwa pia inahimiza ushindani katika utoaji wa huduma kuweza kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na kuchangia ustawi wa wananchi na Taifa.
Mada zilizofundishwa ni maudhui ya habari na utangazaji,masuala leseni na kanuni,taratibu na sheria za uchaguzi.

.jpg)



