-Yaahidi kuendelea kutoa fedha kuisaidia Tanzania kutatua vikwazo vya ukuaji uchumi.
Shirika la Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Corporation-MCC) la Serikali ya Marekani limeeleza kuridhishwa kwake na mageuzi ya mifumo ya kiutendaji, yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika maeneo mbalimbali ikiwemo uimarishwaji wa demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.
Hayo yamebainishwa wakati wa mkutano uliofanyika kati ya ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ujumbe wa Shirika la Changamoto za Milenia uliofanyika tarehe 17 Oktoba, 2024 jijini Dodoma.
Akizungumza kwenye mkutano huo Bw. Dan Barnes, Mkurugenzi wa Sera na Tathmini wa shirika hilo ambaye pia ameongoza ujumbe wa Marekani kwenye mkutano huo, ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita, wameridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Tanzania ambazo zimechangia kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi nchini.
Pia, katika mkutano huo, Bw. Barnes alieleza kuwa kutokana na kuridhishwa na mageuzi hayo, Bunge la Marekani limeridhia Tanzania kuendelea kunufaika na ufadhili wa Shirika hilo la MCC. Maamuzi hayo yataifaya Tanzania kuendelea kupewa misaada katika shughuli za maendeleo ambazo zitasaidia kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Hatua hii iliyofikiwa na MCC inatokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kufanya mageuzi na maboresho katika utendaji wake. Pamoja na sera madhubuti na uongozi thabit wa Serikali, mageuzi hayo yamefikiwa kupitia falsafa ya 4Rs ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi mpya iliyoleta mshikamano wa kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini Tanzania. Falsafa hii imesaidia kuwavutia washirika mbalimbali wa maendeleo kote duniani wakiwemo MCC kwa manufaa ya pande zote.