Jumuiya wa wahitimu wa Shule ya Sekondari Milambo (AMSHA) imeanzisha tuzo maalum ijulikanayo kama Tuzo ya Mwalimu ili kuenzi mchango wa Mwalimu Nyerere na walimu wengine wanaofanya kazi yao kwa weledi mkubwa.
Tuzo hiyo imetolewa kwa Mara ya kwanza kwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius kambarage nyerere ikiwa ni kutambua mchango wake kwa Taifa pamoja Tasnia ya ualimu ikiwemo kufundisha katika shule ya Sekondari Mirambo kati ya mwaka 1946 na 1948
Akikabidhi Tuzo hiyo nyumbani kwa Mwalimu Nyerere,Mwitongo wilayani Butiama Mkoani Mara ,Mjumbe wa Bodi ya AMSHA Abdul-Razaq Badru amesema kuwa Tuzo ya Mwalimu itakuwa ikitolewa kila mwaka kwa Mwalimu aliyetoa mchango ulioleta matokeo chanya kwenye Jamii.
Naye mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Derek Murusuri amesema ujio wa tuzo ya AMSHA utakuwa kichocheo kwa wahitimu wengine kuandaa tuzo kama hizo ili kuwapa motisha walimu wengine na kutambua mchango wao kwenye sekta ya elimu.
Mbali na tuzo iliyokabidhiwa kwa familia ya Mwalimu Nyerere, wajumbe wa AMSHA pia walitoa zawadi mbalimbali kwa shule ya Milambo Sekondari ambazo zitasaidia kuchochea ari ya kujifunza na kupata elimu masafa na taarifa mbalimbali.
Akipokea Tuzo hiyo,Mtoto wa Baba wa Taifa Madaraka Nyerere amewashukuru wanajumuiya mbalimbali ikiwemo umoja wa wahitimu wa sekondari ya Mirambo kwa kutambua na kuthamini mchango wa Mwalimu Nyerere katika ujenzi wa Taifa
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Sheria na Katiba ambaye pia ni Mbunge wa Butiama Jumanne Sagini ambaye aliushukuru uongozi wa AMSHA kwa kubuni tuzo hiyo na uamuzi wake wa kuikabidhi kwa familia ya Mwalimu Nyerere.
"Ninawashukuru sana wana AMSHA kwa kubuni jambo hili na natoa wito kwa wahitimu wengine kukumbuka kurudisha japo kidogo kwenye shule walizosoma," amesema.