Huduma ya Psssf kidijitali yarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama

GEORGE MARATO TV
0


 Idadi ya wanachama wa mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa umma(PSSSF)waliowasilisha maombi ya mafao kwa njia ya kidijitali nchini imeongezeka kutoka mia sita Juni mwaka huu hadi kufikia 8,760 septemba 30 mwaka huu.

Meneja uhusiano wa Mfuko wa Psssf Yesaya Mwakifulefule amesema kuwa ongezeko hilo limefikiwa baada ya wanachama kuhamasishwa kujiunga pamoja na kutumia huduma za Psssf kidijitali.

Akizungumza wakati wa kilele cha maonesho ya saba ya madini Mkoani Geita,Mwakifulefule amesema kuwa ongezeko hilo pia ni matunda ya kampeni ya twende kidijitali iliyomalizika mwezi uliopita.

‘’Hatusubiri mpaka Mwanachama astaafu ndipo tuweze kuwafundisha namna ya kutumia njia ya kidijitali,wapo wanaoelekea kustaafu kati ya miezi sita mpaka miaka 55,hao tunawapa semina za kustaafu,Lakini pia kupitia maonesho kama haya huwa tunawafundisha namna ya kujiunga pamoja na kuwaeleza namna ya kutumia njia hizo”alisema Mwakifulefule

Aidha amebainisha kuwa Mfuko wa Psssf hivi sasa unatoa mafao ndani ya muda wa siku 60 tangu kupokea faili la mstaafu ikiwa nyaraka zote zilizowasilishwa ni sahihi.

Meneja uhusiano wa Mfuko wa Psssf Yesaya Mwakifulefule pia amewatahadharisha wastaafu dhidi ya uwepo wa vitendo vya utapeli vinavyofanywa na watu wasiowaaminifu na kuwaasa kutozifanyia kazi ujumbe mfupi wa maneno(Sms)unaotumwa kupitia namba za watu binafsi.

“Sisi tuna namba zetu maalum lakini pia tuna namba ambazo wanapiga bure,tunawaomba wazitumie ili kuepuka kuangukia mikononi mwa matapeli”alisema Mwakifulefule.

Naye Kaimu meneja wa Mfuko wa Psssf kanda ya ziwa magharibi Thomas Labi amesema kuwa mfuko huo umetumia maonesho hayo kutoa elimu ya hifadhi ya Jamii pamoja na kutoa huduma mbalimbali ikiwemo Pssf kidijitali

‘’katika kipindi hiki tumehakikisha wanachama wengi wamejisajili kwenye mfumo huo na wameweza kutumia na wengi wamerudi kutueleza kwamba huduma hii imekuwa ni rafiki sana kwao na kupunguza ulazima wa wao kufika ofisi za kanda na mikoa kwa ajili ya kupata huduma,kwa sasa wanaweza kujisajili kwenye mfuko pamoja na kuwasilisha madai yao kupitia huduma ya Psssf member portal’’alisema Labi na kuongeza kuwa

‘’Pia kuna huduma ya Psssf kiganjani inayowezesha wanachama kuangalia michango yao kupitia huduma hii,lakini pia wastaafu wanaweza kujihakiki kupitia Psssf kiganjani bila kulazimika kufika katika ofisi za mfuko’’

Kwa upande wake,Mmoja wa wanachama wa Mfuko wa Pssf Posian Matias ameeleza kufurahishwa na maboresho ya huduma za mfuko huo ambapo maboresho hayo yamewaondolea adha ya kulazimika kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kupata taarifa zake kwenye ofisi za mfuko.

”Sasa hivi hata nikiwa chumbani kwangu naweza kupata huduma baada ya kuunganishwa na nimejionea mwenyewe na sio hadithi,nimeunganishwa hapa hapa na nikaweza kuingia kwenye Psssf portal na nikaweza kuona taarifa zangu ikiwemo michango yangu yote,kwa hiyo imeniondolea gharama za kusafiri kwenda kufuatilia taarifa zangu”alisema Posian

Aidha amewahimiza wanachama kubadilika kwa kujiunga na mfumo huo ili kuweza kupata taarifa zao badala ya kuhadaika na matapeli mtaani. 













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top