Hofu na wasiwasi ya wakazi ya kijiji hicho unatokana na uwepo wa mgogoro wa mpaka baina ya kijiji hicho pamoja na kijiji Jirani cha Mikomariro kilichoko kata ya Mihingo wilayani Bunda.
Uvamizi na uporaji wa mifugo unadaiwa kutekelezwa na baadhi ya wananchi wa kijiji jirani cha Mikomariro kwa nia ya kuwashinikiza wenzao wa kijiji cha remng’orori kuhama kutoka kwenye eneo lenye mgogoro.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara,wananchi wa Remng’orori wamesema kuwa mgogoro huo umeathiri ustawi wao kutokana na wengi wao kuibiwa mifugo ikiwemo Maelfu ya ng’ombe,Kondoo na Mbuzi,kufyekewa mazao mashambani huku wengine wakijeruhiwa na kupoteza maisha.
“Tuna njaa kwa sababu hatulimi kwa ukamilifu,kila tukilima watu wa Mikomariro wanavamia mashamba yetu na kuyafyeka mazao yetu,wanatunyang’anya vifaa vya kilimo ikiwemo Majembe na wengine wamechomewa nyumba na kuibiwa mifugo”alisema Godfrey Mokili Mmoja wa wakazi wa remng’orori.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha remng’orori Hezron Msamba ameiomba serikali kuingilia kati ili kuwezesha kupatikana kwa suluhu ya kudumu ya mgogoro huo.
Msamba amesema kuna viashiria vya uvunjifu wa Amani ambazo zimeanza kujitokeza kutoka mikomariro ikiwemo uvamizi na wizi wa mifugo kutoka kwa baadhi ya wakazi wa kijiji chake na kuitaka serikali kuchukua hatua madhubuti hasa wakati huu wa kuelekea msimu wa kilimo.
‘’sisi tunapenda Amani ila hatupo tayari kuona wenzetu wakichomewa nyumba na kuuwa,kuzuiwa kulima pamoja na kuibiwa kwa mifugo yao,Tunaomba mgogoro huu ufike mwisho’’alisema Msamba
Eneo lenye mgogoro lina ukubwa ekari 3,535 na linatumika kwa ajili ya makazi pamoja na malisho ya mifugo ambapo kijiji cha remng’orori kinadai kulimiliki toka enzi za mababu.
Mgogoro huo uliibuka mwaka 2018 ukihusisha vijiji vitatu vya remng’orori wilayani Serengeti,mikomariro wilayani Bunda pamoja na sirorisimba wilayani Butiama na kusababisha maafa ikiwemo vifo na uharibifu wa mali.
Serikali ya mkoa wa mara ilitatua mgogoro huo na kuwapa haki ya umiliki wa eneo hilo Wananchi remng’orori ambapo wananchi wa sirorisimba waliridhia uamuzi huo huku wananchi wa mikomariro wakiupinga na kusababisha kuendelea kwa mgogoro ambapo kilio cha wananchi ni serikali kuu kuingilia kati.





