Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mkombozi iliyopo Mkoani Iringa wametakiwa kukamilisha ujenzi wa Skimu hiyo ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao.
Agizo hilo limetolewana Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji(NIRC)Raymond Mndolwa wakati wa vikao kazi baina ya Uongozi wa Tume hiyo na Wakandarasi hao Mkoani Iringa.
Mndolwa amewataka wakandarasi wa kampuni ya ndani ya Cimfix&engineering pamoja na Kampuni ya CRJE ya nchini China wanaotekeleza wa Mradi wa ujenzi wa Skimu ya Mkombozi kufanya kazi usiku na mchana ili kuwezesha mradi huo kukamilika kwa wakati na hatimaye kuwezesha uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali kunufaisha wakulima kuanzia Msimu Ujao wa Kilimo.
Katika vikao Kazi hivyo,Wakandarasi waliwasilisha mkakati wa kumaliza mradi kwa wakati ikiwemo kuhakikisha kazi zilizosalia zinakamilika oktoba 30 Mwaka huu.
Wajumbe walipitia mkakati huo na kutoa maoni na maazimio, huku mkandarasi akikubali kufanya marekebisho ya mpango kazi ili kuendana na mabadiliko yaliyojadiliwa.
Mradi wa Mkombozi unatekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, kupitia Mkandarasi M/S Cimfix&Engineering Co Ltd kwa gharama ya Shilingi Bilioni 56, ambapo eneo la hekari 15,000 litawekewa Miundo mbinu ya umwagiliaji na utanufaisha jumla ya watu 21,206.
Mwisho