Na Helena Magabe, Tarime.
Waandishi wametakiwa kuandika habari za kuhamasisha Vijana kupima Afya zao na kujikinga na maambukizi ya Ukimwi (VVU) pamoja na kujiepusha na ndoa za utotoni.
Wito huo umetolewa kwenye mafunzo ya siku moja yaliyofanyika katika ukumbi wa Blue sky hotel ambayo yameandaliwa na shirika la utu wa mtoto (CDF) kwa ajili ya kuwajengea uwezo Waandishi wa habari kuandika habari za Afya ya uzazi na Ukimwi.
Afisa miradi wa CDF Anold Masawe ambaye ni mratibu wa mradi wa huduma ya bora za Afya ya uzazi Kwa Vijana amesema vijana ni nyenzo muhimu kuhabarishwa na athari za VVU pamoja na kujiepusha na ndoa na mimba za utotoni.
Amesema elimu inatolewa katika vituo vya Afya 10 na Kata 9 katika Halmashauri ya Tarime Vijijini na tayari vijana 40 wamefundishwa elimu ya afya ya uzazi na VVU ambapo wanatakiwa kuwafikia Vijana 1000 kabla ya mradi huu kuisha ambao ni miaka minne na umebakiza mwaka mmoja.
Mratibu wa Mama Halmashauri ya Wilaya Tarime Beatrice Luomba amewaomba Waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kuandika habari ambazo zitahamasisha vijana kupika Afya zao za uzazi na kujilinda na magonjwa ya zinaa na Ukimwi.
![]() |
Amesema tatizo kubwa na changamoto kubwa kwenye Wilaya ya Tarime ni mimba na ndoa za utotoni hivyo waandishi wanatakiwa kuandika habari juu ya madhara ya ndoa na mimba za utotoni sambamba na kupima Afya zao na kujitambua na kujilinda kupata maambukizi ya VVU.
Leah Daniel ni Mratibu wa huduma ya uzazi na Mtoto Mkoa wa Mara amesema chanzo cha maambukizi ya Ukimwi Kwa Vijana ni ushawishi wa Watu wenye pesa pamoja na Watu wazima ambao tayari wanaishi na maambukizi ya Ukimwi.
Amesema uzazi salama ni hali ya kuwa salama kiafya,kiakili ,kimwili na kijamii hivyo kila mmoja ana wajibu Kwa nafasi yake kuwalinda vijana kuepukana na tabia hatarishi zinazoweza kuwapelekea kupata maambukizi ya Ukimwi pamoja na ndoa za utotoni.